Kabla ya kutoa taarifa hiyo, nianze kuwashukuru ndugu waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali, mashabiki wa muziki na wadau wengine popote mlipo kwa mchango wenu kwangu na kwa wasanii wenzangu, mchango ambao umenifanya mimi kuwepo hapa leo kuweza kuzungumza ninayokusudia kufanya sasa.
Muziki wetu umepiga hatua ukilinganisha na mwanzo kutokana na hali ya kukubaliana na kuheshimiana katika jamii yetu. Hali hii imesaidia pia kutufanya wasanii wa Tanzania kubakia tunaothaminiana na kuheshimiana, huku tukishirikiana katika mazingira mbalimbali.
Ushirikiano huo, kwangu umenisaidia sana. Hivi karibuni umesaidia kunipa tuzo ya wimbo bora wa mwaka katika Hip Hop. Ni ushirikiano huu ambao unanifanya kuja hapa kuusisitiza baada ya kubaini kuwepo hali inayoweza kuchangia kuuvuruga miongoni mwetu.
Kwa kipindi kirefu nimekuwa katika kundi la East Coast Team.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo hali isiyonipa faraja na furaha, hali inayoonyesha kupunguza mshikamano na ushirikiano kati ya wasanii, jambo ambalo binafsi sipendi kuliona likifanyika na kuendelea.
Hali ya kushambuliana kwa maneno katika kazi za kisanii ilishaanza kupotea baada ya kutugharimu sana. Muziki wetu ulishaanza kuwa na dira ya kutazama mbele, lakini nionavyo kuna hali nyingine imeanza kutuandama.
Hali hiyo nionavyo inaweza kutufanya kufarakana na hivyo kuwaudhi mashabiki wetu. Ikumbukwe kuwa, mashabiki wetu wako katika maeneo mbalimbali na wanaishi maisha ya daraja zote yaani za juu, kati na chini.
Nimekuja kuwaambia uamuzi nilioufanya, kwa utaratibu mzuri kabisa huku nikiwa na asilimia mia moja ya nia njema, baada ya kufikiri na kupima kwa muda uamuzi huo.
The Then East Coast Team - Sherif, Snare, AY and Mwana FA
Kwa kipindi kirefu nimekuwa katika kundi la East Coast Team.Nadhani wengi wenu mnalijua na kulitambua hilo.
Leo naomba niwatangazie rasmi kwamba NIMEJITOA KATIKA KUNDI LA EAST COAST TEAM. Sababu kubwa ya kufanya hivi ni kutokana na kazi zangu binafsi kunihitaji zaidi ya kuwa katika kundi na pia kutazama mazingira bora ya maslahi.
East Coast Team tangu inaanzishwa mimi ni miongoni wa waanzilishi,na tulishirikiana bega kwa bega katika kila hali.Sasa ECT si kundi tena ni KAMPUNI.Lakini kitu ambacho kilinivunja moyo ni kuwa kisheria na taratibu katika kuanzisha kampuni ni lazima kuwe na WANAHISA.Sasa cha kushangaza katika majina ya wanahisa wa kampuni ya ECT mimi kama mmoja wa waanzilishi na nguzo imara ya ECT nilingundua jina langu halipo na yamewekwa majina mengine.Kwa haraka haraka unagundua kuwa sitakuwa na haki kamili katika kampuni.
Kutokana na hali hiyo nilivunjika moyo.Na katika kutazama sana niliona kama nitapata kipindi cha kufanya kazi zangu kama mimi mafanikio ya karibu kabisa nitayapata kuliko ilivyo sasa.
Sijafanya maamuzi haya kwa chuki na kundi, hapana ni kutazama namna njema ya kusaka mafanikio. Bado nina urafiki wa damu na ECT na nitabakia kuwatakia mafanikio kama ambavyo na wao watatakiwa kunifanyia.
Kukitokea lolote tutashirikiana na tutaendelea kuwa ndugu daima, naomba muelewe hivyo, narudia tena kusisitiza amani na upendo baina yetu sisi kama vijana na wasanii kwa ujumla.
NAWASHUKURU SANA KWA KUSOMA HABARI HII.BADO NAHITAJI SUPPORT YENU KWA HALI NA MALI NA NAWAAHIDI SITAWAANGUSHA!!
AMBWENE YESSAYAH (A.Y)


